Sunday, July 10, 2011

BUNGE LA KUNWA NA VITAMBULISHO VYA TAIFA

Na Mwandishi Wetu

   
BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeridhishwa na uwezo wa kiteknolojia alionao mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kutengeneza Vitambulisho vya Taifa.


RAi hiyo ilitolewa na timu ya wabunge waliotembelea Kampuni ya Iris Corporation Berhad ya Malaysia iliyoshinda zabuni ya kutengeneza Vitambulisho vya Taifa, jana walipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam.


Akizungumzia ziara hiyo, Mkuu wa Msafara huo, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Anna Abdallah alisema Serikali imechelewa kutoa Vitambulisho vya Taifa hivyo haina budi kuharakisha mchakato huo kwa sababu vina faida nyingi kwa ustawi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii Tanzania.

“Sisi wabunge tunasema Vitambulisho vya Taifa ni lazima vitolewe haraka kwa sababu ni muhimu kutambuana, huwezi kumtofautisha mtanzania na watu wa mataifa mengine kwa rangi au sura tu, Lazima tuwe na Vitambulisho vya Taifa,
“wenzetu Malaysia wanatoa vitambulisho hata kwa watoto wadogo kwa nini sisi tushindwe,” alisema.


Akizungumzia kuhusu Kampuni ya Iris alisema, “Ni kampuni namba moja duniani kutengeneza vitambulisho vya kisasa. Hata mataifa ya Ulaya yanakwenda kujifunza kwa kampuni hiyo. Tutegemee kitu kizuri,” alisema.

 
Mbunge wa Mlalo (CCM), Brigedia Jenerali mstaafu, Hassan Ngwilizi alisema Kampuni ya Iris ina uwezo mkubwa na italisaidia Taifa kutengeneza Mfumo wa Utambuzi na Usajili wa Watu na hatimaye kutoa Vitambulisho vya Taifa vyenye ubora wa hali ya juu.

Alisema teknolojia itakayotumiwa kutengeneza Vitambulisho vya Taifa na Iris ambayo pia imetumiwa nchini Malaysia ni ya kisasa ambayo inaweza kuhifadhi taarifa nyingi katika kitambulisho kimoja.
“Wenzetu wamepiga hatua, wameweza kuweka hata hati ya kusafiria (Passport) katika Kitambulisho chao cha Taifa,” alisisitiza.
 
Akizungumzia kuhusu mradi wa Vitambulisho vya Taifa, Mbunge wa Maswa (CHADEMA), John Shibuda alisema Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inapaswa kuungwa mkono na kupewa kipaumbele ili ipate fedha na kuanza utekelezaji wa mradi huo.

“Vitambulisho ni mbegu ambayo itazaa matunda mengi, tuiwezeshe NIDA ili tuvune matunda yake haraka. Ni mradi utakaoleta neema kwa sababu ukianza kutekelezwa ndani ya mwaka mmoja tunaweza kupata zaidi ya trilioni mbili.

“Nchi kama Kenya haitegemei wafadhili, wanakusanya kodi inavyopaswa kwa sababu wana Vitambulisho vya Taifa,” alisema.

Wabunge waliozulu Iris Corporation Berhad ni Anna Abdallah ambaye alikuwa kiongozi wa msafara, Brigedia Jenerali mstaafu Ngwilizi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), Betty Machangu (CCM), Moses Machali (NCCR-Mageuzi), Jasson Rweikiza (CCM), Rebecca Mngodo (CHADEMA) na Anastazia Wambura (CCM).

Wengine ni Rachael Mashishanga (CHADEMA), Mohamed Sanya, Mussa Hassan Mussa na John Shibuda.

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ilisaini rasmi mkataba na Mkandarasi, Iris Corporation Berhad ya Malaysia Aprili 21, 2011. Mkataba huu ulitiwa saini na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha kwa niaba ya Serikali.

Mchakato wa kumpata mkandarasi wa Vitambulisho vya Taifa ulivyokuwa
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mei mwaka 2008, ilitangaza zabuni ya kujenga Mfumo wa Taifa wa Utambuzi na Usajili wa Watu.

Baada ya zabuni hiyo kutangazwa kwenye vyombo vya habari, Kampuni mia moja na nne (104) zilijitokeza kununua vitabu vya zabuni

Kati ya Kampuni hizo (104), Kampuni 54 zilirudisha zabuni hizo.

Kamati ya tathmini ya zabuni hii ambayo ilihusisha wataalamu mbalimbali kutoka taasisi mbalimbali za Serikali vikiwemo vyombo vya Ulinzi na Usalama ilikaa na kufanya mchujo wa awali ambapo Kampuni nane (8) zilipita katika mchujo huu, mbili kati ya hizo kwa masharti maalum.

Bodi ya Manunuzi ya Wizara ilipitisha Kampuni sita (6) baada ya zile mbili zilizopewa masharti kushindwa kutimiza masharti hayo.

Kampuni zilizopitishwa ni Unisys – Afrika Kusini, Giesecke & Devrient FZE- UAE, Iris Corporation Berhad – Malaysia, Marubeni Corporation in Joint Venture with Zetes and NEC – Japan, Tata Consultancy Services in Joint Venture with On Track Innovation LTD – India na Madras Security Printers – India

Baadaye Mamlaka ya Usimamizi wa Zabuni za Umma (PPRA) iliamua kufanya uchunguzi wa mchakato wa zabuni hii baada ya kuwapo malalamiko mballimbali toka kwa wananchi kupitia vyombo vya habari.

Katika matokeo ya uchunguzi wake, PPRA ilielekeza Kampuni ya Madras Security Printers iondolewe kwenye mchakato kwa kuwa mbia wake Kampuni ya Bharat Electronics ilikuwa imeingia ubia (Joint Venture) na Kampuni nyingine katika mchakato huu kinyume na masharti yaliyowekwa katika kitabu cha zabuni.

Kampuni tano zilizobaki zilipelekewa “RFP” kwa ajili ya awamu ya pili ya mchujo.

Kampuni tatu kati ya tano zilizobaki zilijitoa katika mchakato kwa hiari na zikabaki Kampuni mbili ambazo ni Iris corporation Berhad na On Track Innovation LTD ambazo zilishindanishwa katika vipengele vya Ufundi/Utaalamu (Technical Evaluation) na Fedha (Financial Evaluation).
Kampuni ya On Track Innovation baada ya kufanyiwa tathmini ilionekana haikuweza kukidhi vigezo vya kiufundi na kiutaalamu vilivyowekwa hivyo basi iliondolewa katika mchakato na kubakiza kampuni moja ya Iris Corporation Berhad.

Baada ya kufanyiwa tathmini ya bei, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa iliunda timu ya kwenda kuifanyia uchunguzi (Post Qualification) Kampuni ya Iris ili kuweza kujiridhisha juu ya uwezo wake wa kutekeleza mradi huu kwa mujibu wa kanuni ya 94 ya GN 97 ya Kanuni za Manunuzi ya Umma, 2005, na Machi 14-16, 2011 timu hiyo ilikwenda Malaysia kufanya uchunguzi.

Timu hii iliundwa na wataalamu kutoka vyombo mbalimballi vya Serikali vikiwamo vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Aidha Mamlaka iliunda kamati ya majadiliano kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma. Kamati hii pia iliundwa na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Wizara ya Fedha pamoja na Ofisi ya Mwnasheria Mkuu wa Serikali.

Majadiliano na Mzabuni huyu yalifanyika kwa muda wa wiki mbili ambapo taarifa ya Kamati hii ilipitiwa na kuridhiwa na Bodi ya Manunuzi ya Mamlaka.
Baada ya Bodi kuridhia taarifa hiyo, Mzabuni huyu alipewa barua ya “award” na kisha rasimu ya Mkataba ikapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Aidha rasimu hii ilipelekwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya fedha kwa ajili ya kuidhinisha kipengele cha msamaha wa kodi kwa bidhaa zote zitakazohusu Mradi huu.

Baada ya kupata idhini ya Ofisi hizi mbili ndipo Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ilisaini rasmi mkataba na Mkandarasi.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment