Monday, April 29, 2013

Lady Jay Dee atuma salamu


Cheka, Mashali kupima uzito
Na Mwali Ibrahim, Dar es Salaam
HOMA ya pambano la kuwania mkanda wa IBF/Afrika na gari aina ya Noah lenye thamani ya Sh milioni 12 kati ya mabondia Francis Cheka na Thomas Mashali, imezidi kupanda, baada ya mabondia hao leo  kupima uzito kwa ajili ya mpambano huo utakaofanyika kesho kwenye Ukumbi wa PTA, Dar es Salaam.
Tayari majaji na marefa kutoka nje ya nchi ambao wanakuja nchini kusimamia mpambano huo, wamewasili nchini kwa ajili ya kumsaka bingwa huyo, ambaye atakuwa kati ya Cheka, ambaye anatetea mkanda huo au Mashali anayeutaka kwa mara ya kwanza.
Refa wa mpambano huo atakuwa John Shipanuka kutoka Zambia, huku majaji wakiwa ni Daudi Chikwanje kutoka Malawi, ambaye ndiye Katibu Mkuu wa Chama cha Ngumi Malawi na ambaye anakuwa jaji namba moja, Steve Okumu wa Kenya, ambaye anakuwa jaji namba mbili na Ismail Sekisambu wa Uganda ambaye anakuwa jaji namba tatu. 
Na kwa upande wa msimamizi wa pambano hilo, atakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Viwango na Ushindi wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Boniface Wambura, ambaye ni Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), atakayesimamia pambano hilo badala ya Rais wa IBF/Afrika Mashariki na Kati, Onesmo Ngowi.
Kwa upande wa  Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO) ambao ni wa simamizi washiriki, Yassin Abdalah ‘Ostadh’ alisema utaratibu na kanuni walizopanga kutumika katika mchezo huo ziko palepale, ikiwa ni pamoja na kupima matumizi ya dawa za kuongeza nguvu na bangi ambapo mabondia wote watapimwa na majibu kutolewa hapo hapo.
“Kama tulivyopanga awali, tunataka pambano hilo kuwa la kimataifa kulingana na hadhi ya ubingwa wenyewe, hivyo mabondia hawa watapimwa matumizi ya dawa hizo na endapo bondia atabainika kutumia atakuwa tayari ameishajitoa katika mpambano na kumuacha mwenzie kutawazwa kuwa bingwa bila kupambana,” alisema.
XXXXXX

Taifa Ngumi kuanza mazoezi Mei 7
Na Mwali Ibrahim, Dar es Salaam
KIKOSI kipya cha Taifa cha Ngumi za Ridhaa kilichotangazwa hivi karibuni na Kocha wa Mkuu wa ngumi hizo, Remmy Ngabo, kinatarajia kuanza mazoezi rasmi Mei 7, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, kujinoa kwa ajili ya mshindano ya Afrika yatakayofanyika Juni 20 hadi 30 nchini Mauritius.
Kikosi hicho cha mabondia 16 wakiwa na makocha tisa, kilitangazwa hivi karibuni ambapo mabondia hao walichaguliwa kupitia mashindano mbalimbali waliyoshiriki hivi karibuni.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Makore Mashaga, alisema  kwa sasa wapo katika mchakato wa kuwaombea ruhusa mabondia ambao ni wafanyakazi wa vyombo vya usalama, ili waweze kupata nafasi ya kuanza mazoezi yao kwa pamoja na mabondia wengine.
“Mazoezi yatakuwa yanafanyika kila siku kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa sita mchana na kwa sasa tunajivunia kuwa na mabondia wengi wenye umri mdogo na wakiwa ni mara ya kwanza kwao kuitwa timu ya Taifa, tuna imani watakuwa na hamu kubwa ya kuiwakilisha vyema timu,” alisema.
XXXXXX

Lady Jay Dee atuma salamu
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MSANII mahiri wa kike katika muziki wa kizazi kipya nchini, Judith Wambura ‘Lady Jay Dee’, ametuma salamu zake kwa mashabiki wa muziki huo, kwa kumuunga mkono tangu alipoanza kazi hiyo miaka 13 iliyopita.
Katika salamu zake hizo alizozitoa Dar es Salaam jana, Jay Dee, alisema ameandaa sherehe za miaka 13 zitakazoambatana na  uzinduzi wa albamu yake ya sita inayoitwa ‘Nothing But The Truth’, iliyo na jumla ya nyimbo 10, itakayofanyika Mei 31 mwaka huu.
Alisema katika sherehe hizo pia kutakuwa na shoo ya  nyimbo zote bora alizoshirikiana na baadhi ya wasanii wenzake nchini.
“Nashukuru Mungu tuko pamoja na pia nashukuru umma wa Tanzania kwa kuendelea kunipa ushirikiano katika muziki wa Tanzania na kunipa nguvu mimi kama msanii.
“Nashukuru vyombo vyote vya habari vinavyoshiriki kikamilifu kukuza na kulinda sanaa ya Tanzania bila kujali maslahi binafsi,” alisema.
XXXXX


Skylight, THT kupamba bonanza Mei Mosi
Na Humphrey Shao, Dar es Salaam
BENDI ya muziki wa dansi ya Skylight na kundi la wasanii kutoka Nyumba ya Vipaji Tanzania (THT), wanatarajia kutoa burudani katika bonanza la Mei Mosi, litakalofanyika katika viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam.
Bonanza hilo limeandaliwa na Clouds FM kupitia kipindi cha Sports Extra kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mratibu wa bonanza hilo, Shafii Dauda, alisema  bonanza hilo linatarajia kushirikisha jumla ya makampuni 14 yaliyotuma maombi ya kushiriki.
“Tulitangaza kupitia vyombo vyetu vya habari kama makampuni yanayotaka kushiriki yajitokeze, hivyo makampuni yaliyojitokeza ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), TCC , Benki  ya CRDB, Simbanet, Shirika la Taifa la Hifadhi  ya Jamii (NSSF), Clouds Media Group, Fastjet, Umoja Water, Infinity, Tanesco na NMB,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa nje wa Vodacom Tanzania, Salum Mwalimu, alisema wameamua kushirikiana na Clouds kwa kuwa wao ni sehemu ambayo wanafikia wateja wao wengi, hivyo hicho wanachofanya ni kwa ajili ya watu na wao wapo kwa ajili ya watu.
XXXXX

Wasanii THT kuachia Ugonjwa wa Moyo
Na Asteria Mdakirwa, Dar es Salaam
WASANII  kutoka Nyumba ya Vipaji Tanzania (THT), Saidi Christopher ‘Muki’ na Fred Felix ‘Fredwayne’ wanatarajia kutoa nyimbo nyingine mpya ijulikanayo kama Ugonjwa wa Moyo mwezi ujao.
Wasanii hao awali walitoka na nyimbo ya Kibega, wameamua kuja kivingine zaidi na wimbo huo uliotengenezwa katika Studio ya Surround Sound, chini ya Emma The Boy.
Ugonjwa wa Moyo ni wimbo ulio katika hadhi na maadili ambayo kila shabiki ataifurahia kutokana na kuimbwa katika lugha ya Kiswahili na Kikongo, huku ikitengenezwa katika kiwango cha hali ya juu.
XXXXXXMWISHO.

Baadhi ya wachezaji wa timu ya Yanga, wakifanya mazoezi Kwenye Uwanja wa Bora Kijitonyama Dar es Salaam hivi karibuni. Yanga kesho inacheza na Coast Union kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Brandts aisoma Simba dakika 45
*Asema hawana kitu, ni warahisi sana watakiona Mei 18
*Ashangaa Yanga walifungwaje 5-0, awatoa hofu mashabiki
Na Humphrey Shao, Dar es Salaam

DAKIKA 45 zilitosha kumuondoa uwanjani Kocha wa Yanga, Ernest Brandts, baada ya kuona zinatosha kuisoma timu ya Simba pindi ilipokuwa ikicheza na Polisi Morogoro, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Brandts ambaye aliwasili katika mchezo huo  dakika kumi kabla ya mchezo kuanza, akiongozana na mmoja wa watumishi wa klabu hiyo na kuketi jukwaa kuu, alikuwa ameshika ‘notebook’ akiandika kila  kinachojiri katika mchezo huo.
Kocha huyo alipata nafasi ya kushuhudia ni jinsi gani Simba ikicheza, hadi kuona namna walivyoweza kufanya makosa na kupachikwa bao la mapema kabla ya kusawazisha, lakini aliondoka baada ya kumalizika kipindi cha kwanza, ili aweze kuendelea na majukumu mengine.
MTANZANIA ilifanya jitihada na hatimaye kupata nafasi kuzungumza na kocha huyo, akiwa ndani ya gari yake aina ya Prado wakati akijiandaa kuondoka uwanjani hapo, na kumuuliza kwanini anaondoka mapema uwanjani na kujibu tayari amekipata alichokuwa anakitaka kutoka kwa wapinzani wake.
“Sioni sababu ya kuendelea kukaa hapa wakati kazi iliyonileta hapa nimemaliza, naendelea na programu nyingine kwani nimewaona Simba wakicheza na kwangu sio tishio wanacheza rahisi sana kuliko nilivyofikiri na wachezaji wangu, naamini nitawafunga tu.
 “Nakumbuka mara ya kwanza nilipopewa majukumu ya kuinoa timu hii, nilipewa habari za wapinzani wetu kutufunga bao 5-0 msimu uliyopita, sikuliweka akilini kwakuwa nilikuwa nataka timu ifanye vizuri kwanza na imekuwa hivyo, sasa tutakutana Mei 18,” alisema Brandts.
Mholanzi huyo alisema, Simba wamepoteza kiwango kabisa, hata wale wachezaji vijana ambao wamepewa nafasi katika timu hiyo, bado hawajaizoea ligi vizuri, hivyo udhaifu huo utaisadia timu yake kushinda katika mechi hiyo.
Alisema kikosi chake kimeimarika, wachezaji wake hawatacheza kwa presha kwani tayari kombe wanalo, wanachotakiwa kufanya ni kurudisha heshima ambayo waliipoteza, ambapo walifungwa na kunyang’anywa kombe.

“Nimewaona Simba nitakwenda kufanyia kazi mapungufu yao, ambayo yamejitokeza ili kuweza kuimarisha kikosi kiweze kuwasambaratisha Simba ipasavyo, mashabiki wategemee ushindi hakuna tena 5-0,” alisema.
Aliongeza kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya kuivaa Coastal Union kesho na kuondoka na pointi tatu muhimu, licha ya timu yake kutangazwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara, hivyo hakutakuwa na kigezo cha kupoteza mechi hata moja kati ya hizo zilizosalia.

The Keri Christy, (singing); and Jeff Hoffman, (playing guitar); Jazz Duo perform a concert at the Alliance Francaise recently. (Photo courtesy of American Embassy)




Tuesday, April 23, 2013

VIJANA WA KEJO WAMAUA KUJENGA DARAJA KATIKA MFREJEI WA MOLEMO

Vijana wa kikundi cha mazoezi cha Keko Joging Community (KEJO)wakiwa katika ujenzi wa Daraja la mfereji wa molemo amablo lilikuwa limebomolewa na mafuriko ya mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam, ujenzi huo ni sehemu ya kuhamasisha watu kujiunga na mazoezi kwa afaya yao na kuondoa dhana ya mazoezi ni uhuni . Picha na Humphrey Shao.

Thursday, April 18, 2013

BONDIA FADHILI MAJIHA ARUDI NA UBINGWA KUTOKA INDONESIA BAADA YA KUMDUNDA Heri Amol

Bondia Fadili Majia akiwa na kombe la ubintaifa wa wa ngumi kimaifa alililinyakua nchini Indonesia wiki iliyopita alipo mpiga bondia Heri Amol  hapa alipo rakiwa baada ya kurudi dar es salaam jana kutoka kushoto ni Kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini wengine ni mabondia Japhet Kaseba, Kanda Kabongo na Pendo Njau picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com

NGUMI KUPIGWA CHALINZE

Mabondia Mwaite juma,cosmas kibuga na shabani kaoneka ni baadhi ya mabondia wa dar es salaam watakaokwenda chalinze kuhamasisha ngumi za kulipwa wilayani humo kwa kuzipiga na mabondia wakali wa chalize.
Kampuni inayoandaa mapambano kwa ajili ya kunyanyua vipaji vya mabondia machipukizi ya Bigright Promotion, imaeandaa pambano hilo ili kutanua wigo wa michezo nchini kwa kuanzia kutembelea wilaya zinazohamasika kimchezo ikiwemo chalinze.
Tumeamua kufanya chalinze kwa sababu tunataka chalinze iwe ndio mfano kwa kuandaa pambano hili ambalo litawakutanisha chipukizi wakali wa dar na wakali wa chalinze,pia kutakuwepo na mapambano mengine yenye ushindani wa hali ya juu na vituko kama vile la Pius puto atakaezipiga na iddi mkatatiketi -hawa ni mbabe wa sokoni na mbabe wa stendi watazipiga kumaliza ubishi wao uliotanda kwa muda mrefu. ukiondoa pambano hilo Minyusi abdala atazipiga na shaban kaoneka, Baraka nuhu"chalinze hamjambo" atazipiga na goodluck suleiman, alex kdo atazipiga na herman shekivuli, iddi mwera atazipiga na ramadhan misugwa na mapambano mengineyo mengi likiwemo la ustadh mwenye msimamo mkali ustadh Kurasheni aliyeahidi kuchinja kama anachinja kondoo ulingoni atakaezipiga na makali wa bodaboda mzee kachacha.mgeni rasmi wa pambano hilo atakuwa ni diwani wa  Chalinze bwilingu bw naser Karama ambaye muda wote amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha vijana kushiriki michezo na ametoa basi kubwa kwa ajili ya mashabikitoka daresslaam kwenda kushangilia na kurudi.
wakati huohuo diwani Karama anategemea kujenga ukumbi mkubwa wangumi hapo chalinze, hivyo ngumi zote za kimataifa zitakuwa zikipigwa hapo