Monday, April 29, 2013

Lady Jay Dee atuma salamu


Cheka, Mashali kupima uzito
Na Mwali Ibrahim, Dar es Salaam
HOMA ya pambano la kuwania mkanda wa IBF/Afrika na gari aina ya Noah lenye thamani ya Sh milioni 12 kati ya mabondia Francis Cheka na Thomas Mashali, imezidi kupanda, baada ya mabondia hao leo  kupima uzito kwa ajili ya mpambano huo utakaofanyika kesho kwenye Ukumbi wa PTA, Dar es Salaam.
Tayari majaji na marefa kutoka nje ya nchi ambao wanakuja nchini kusimamia mpambano huo, wamewasili nchini kwa ajili ya kumsaka bingwa huyo, ambaye atakuwa kati ya Cheka, ambaye anatetea mkanda huo au Mashali anayeutaka kwa mara ya kwanza.
Refa wa mpambano huo atakuwa John Shipanuka kutoka Zambia, huku majaji wakiwa ni Daudi Chikwanje kutoka Malawi, ambaye ndiye Katibu Mkuu wa Chama cha Ngumi Malawi na ambaye anakuwa jaji namba moja, Steve Okumu wa Kenya, ambaye anakuwa jaji namba mbili na Ismail Sekisambu wa Uganda ambaye anakuwa jaji namba tatu. 
Na kwa upande wa msimamizi wa pambano hilo, atakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Viwango na Ushindi wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Boniface Wambura, ambaye ni Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), atakayesimamia pambano hilo badala ya Rais wa IBF/Afrika Mashariki na Kati, Onesmo Ngowi.
Kwa upande wa  Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO) ambao ni wa simamizi washiriki, Yassin Abdalah ‘Ostadh’ alisema utaratibu na kanuni walizopanga kutumika katika mchezo huo ziko palepale, ikiwa ni pamoja na kupima matumizi ya dawa za kuongeza nguvu na bangi ambapo mabondia wote watapimwa na majibu kutolewa hapo hapo.
“Kama tulivyopanga awali, tunataka pambano hilo kuwa la kimataifa kulingana na hadhi ya ubingwa wenyewe, hivyo mabondia hawa watapimwa matumizi ya dawa hizo na endapo bondia atabainika kutumia atakuwa tayari ameishajitoa katika mpambano na kumuacha mwenzie kutawazwa kuwa bingwa bila kupambana,” alisema.
XXXXXX

Taifa Ngumi kuanza mazoezi Mei 7
Na Mwali Ibrahim, Dar es Salaam
KIKOSI kipya cha Taifa cha Ngumi za Ridhaa kilichotangazwa hivi karibuni na Kocha wa Mkuu wa ngumi hizo, Remmy Ngabo, kinatarajia kuanza mazoezi rasmi Mei 7, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, kujinoa kwa ajili ya mshindano ya Afrika yatakayofanyika Juni 20 hadi 30 nchini Mauritius.
Kikosi hicho cha mabondia 16 wakiwa na makocha tisa, kilitangazwa hivi karibuni ambapo mabondia hao walichaguliwa kupitia mashindano mbalimbali waliyoshiriki hivi karibuni.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Makore Mashaga, alisema  kwa sasa wapo katika mchakato wa kuwaombea ruhusa mabondia ambao ni wafanyakazi wa vyombo vya usalama, ili waweze kupata nafasi ya kuanza mazoezi yao kwa pamoja na mabondia wengine.
“Mazoezi yatakuwa yanafanyika kila siku kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa sita mchana na kwa sasa tunajivunia kuwa na mabondia wengi wenye umri mdogo na wakiwa ni mara ya kwanza kwao kuitwa timu ya Taifa, tuna imani watakuwa na hamu kubwa ya kuiwakilisha vyema timu,” alisema.
XXXXXX

Lady Jay Dee atuma salamu
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MSANII mahiri wa kike katika muziki wa kizazi kipya nchini, Judith Wambura ‘Lady Jay Dee’, ametuma salamu zake kwa mashabiki wa muziki huo, kwa kumuunga mkono tangu alipoanza kazi hiyo miaka 13 iliyopita.
Katika salamu zake hizo alizozitoa Dar es Salaam jana, Jay Dee, alisema ameandaa sherehe za miaka 13 zitakazoambatana na  uzinduzi wa albamu yake ya sita inayoitwa ‘Nothing But The Truth’, iliyo na jumla ya nyimbo 10, itakayofanyika Mei 31 mwaka huu.
Alisema katika sherehe hizo pia kutakuwa na shoo ya  nyimbo zote bora alizoshirikiana na baadhi ya wasanii wenzake nchini.
“Nashukuru Mungu tuko pamoja na pia nashukuru umma wa Tanzania kwa kuendelea kunipa ushirikiano katika muziki wa Tanzania na kunipa nguvu mimi kama msanii.
“Nashukuru vyombo vyote vya habari vinavyoshiriki kikamilifu kukuza na kulinda sanaa ya Tanzania bila kujali maslahi binafsi,” alisema.
XXXXX


Skylight, THT kupamba bonanza Mei Mosi
Na Humphrey Shao, Dar es Salaam
BENDI ya muziki wa dansi ya Skylight na kundi la wasanii kutoka Nyumba ya Vipaji Tanzania (THT), wanatarajia kutoa burudani katika bonanza la Mei Mosi, litakalofanyika katika viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam.
Bonanza hilo limeandaliwa na Clouds FM kupitia kipindi cha Sports Extra kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mratibu wa bonanza hilo, Shafii Dauda, alisema  bonanza hilo linatarajia kushirikisha jumla ya makampuni 14 yaliyotuma maombi ya kushiriki.
“Tulitangaza kupitia vyombo vyetu vya habari kama makampuni yanayotaka kushiriki yajitokeze, hivyo makampuni yaliyojitokeza ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), TCC , Benki  ya CRDB, Simbanet, Shirika la Taifa la Hifadhi  ya Jamii (NSSF), Clouds Media Group, Fastjet, Umoja Water, Infinity, Tanesco na NMB,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa nje wa Vodacom Tanzania, Salum Mwalimu, alisema wameamua kushirikiana na Clouds kwa kuwa wao ni sehemu ambayo wanafikia wateja wao wengi, hivyo hicho wanachofanya ni kwa ajili ya watu na wao wapo kwa ajili ya watu.
XXXXX

Wasanii THT kuachia Ugonjwa wa Moyo
Na Asteria Mdakirwa, Dar es Salaam
WASANII  kutoka Nyumba ya Vipaji Tanzania (THT), Saidi Christopher ‘Muki’ na Fred Felix ‘Fredwayne’ wanatarajia kutoa nyimbo nyingine mpya ijulikanayo kama Ugonjwa wa Moyo mwezi ujao.
Wasanii hao awali walitoka na nyimbo ya Kibega, wameamua kuja kivingine zaidi na wimbo huo uliotengenezwa katika Studio ya Surround Sound, chini ya Emma The Boy.
Ugonjwa wa Moyo ni wimbo ulio katika hadhi na maadili ambayo kila shabiki ataifurahia kutokana na kuimbwa katika lugha ya Kiswahili na Kikongo, huku ikitengenezwa katika kiwango cha hali ya juu.
XXXXXXMWISHO.

No comments:

Post a Comment