Brandts aisoma Simba dakika 45
*Asema
hawana kitu, ni warahisi sana
watakiona Mei 18
*Ashangaa
Yanga walifungwaje 5-0, awatoa hofu mashabiki
Na Humphrey
Shao, Dar es Salaam
DAKIKA 45 zilitosha
kumuondoa uwanjani Kocha wa Yanga, Ernest Brandts, baada ya kuona zinatosha
kuisoma timu ya Simba pindi ilipokuwa ikicheza na Polisi Morogoro, katika
mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Brandts
ambaye aliwasili katika mchezo huo
dakika kumi kabla ya mchezo kuanza, akiongozana na mmoja wa watumishi wa
klabu hiyo na kuketi jukwaa kuu, alikuwa ameshika ‘notebook’ akiandika kila kinachojiri katika mchezo huo.
Kocha huyo
alipata nafasi ya kushuhudia ni jinsi gani Simba ikicheza, hadi kuona namna
walivyoweza kufanya makosa na kupachikwa bao la mapema kabla ya kusawazisha,
lakini aliondoka baada ya kumalizika kipindi cha kwanza, ili aweze kuendelea na
majukumu mengine.
MTANZANIA
ilifanya jitihada na hatimaye kupata nafasi kuzungumza na kocha huyo, akiwa
ndani ya gari yake aina ya Prado wakati akijiandaa kuondoka uwanjani hapo, na
kumuuliza kwanini anaondoka mapema uwanjani na kujibu tayari amekipata
alichokuwa anakitaka kutoka kwa wapinzani wake.
“Sioni
sababu ya kuendelea kukaa hapa wakati kazi iliyonileta hapa nimemaliza, naendelea
na programu nyingine kwani nimewaona Simba wakicheza na kwangu sio tishio
wanacheza rahisi sana
kuliko nilivyofikiri na wachezaji wangu, naamini nitawafunga tu.
“Nakumbuka
mara ya kwanza nilipopewa majukumu ya kuinoa timu hii, nilipewa habari za wapinzani
wetu kutufunga bao 5-0 msimu uliyopita, sikuliweka akilini kwakuwa nilikuwa
nataka timu ifanye vizuri kwanza na imekuwa hivyo, sasa tutakutana Mei 18,” alisema
Brandts.
Mholanzi huyo alisema, Simba wamepoteza kiwango
kabisa, hata wale wachezaji vijana ambao wamepewa nafasi katika timu hiyo, bado
hawajaizoea ligi vizuri, hivyo udhaifu huo utaisadia timu yake kushinda katika
mechi hiyo.
Alisema kikosi chake kimeimarika, wachezaji wake
hawatacheza kwa presha kwani tayari kombe wanalo, wanachotakiwa kufanya ni
kurudisha heshima ambayo waliipoteza, ambapo walifungwa na kunyang’anywa kombe.
“Nimewaona
Simba nitakwenda kufanyia kazi mapungufu yao,
ambayo yamejitokeza ili kuweza kuimarisha kikosi kiweze kuwasambaratisha Simba ipasavyo,
mashabiki wategemee ushindi hakuna tena 5-0,” alisema.
Aliongeza
kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya kuivaa Coastal Union kesho na kuondoka na
pointi tatu muhimu, licha ya timu yake kutangazwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara,
hivyo hakutakuwa na kigezo cha kupoteza mechi hata moja kati ya hizo zilizosalia.
No comments:
Post a Comment