SERIKALI imetakiwa kuacha kuiingilia kazi za Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na badala yake iwape uhuru wa kufanyakazi hiyo kwa ufasaha
na kuandaa katiba wanayoitaka wananchi.
Hayo yamesemwa jana na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph
Sinde Warioba wakati wa uzinduzi wa tume hiyo na kukabidhiwa jengo la kufanyia
kazi hiyo.
Mwenyekiti huyo amesema isije ikafika wakati tume ikashindwa
kufanyakazi ipasavyo kwa sababu ya maslahi ya watu wachache kwani kufanya hivyo
itakuwa ni kuingilia uhuru wa tume na kuwanyima haki wananchi ya kupendekeza
katiba waipendayo.
“ Nyie mliotuchagua tunaomba tafadhari mtupe nafasi isije
ikaja leo au kesho mnaanza kutusumbua tupindishe kilichopo kwa madai mna watu
wenu ndani ya tume naomba ieleweke kuwa tume si ya kikundi fulani ni ya
wananchi hivyo hatutaki kufanyakazi kwa
presha ya watu fulani,”amesema Warioba.
Amesema kazi waliyopewa ni ngumu hivyo wana imani serikali
itawapa ushirikiano wa kuwafikia wananchi wote ili waweze kutoa maamuzi yao na kuandaa katiba
yenye maslahi ya umma.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
amesema Serikali imeandaa mazingira safi
ya kuhakikisha tume hiyo inafanyakazi kwa ufanisi zaidi.
Amesema kuwa serikali
imetekeleza ahadi aliyoitoa rais alipoiapisha tume hiyo Aprili 13 mwaka huu ya
kuhakikisha tume hiyo inafanyakazi kwenye mazingira stahiki yenye ulinzi wa
kutosha, usalama , na vifaa vya mawasiliano na vya kutunzia kumbukumbu vya
kisasa.
Pia serikali imenunua magari 30, kwa ajili ya tume hiyo ili
kuweza kuwafikia wananchi kwa urahisi na kuepuka vikwazo katika utendaji wa
kazi hiyo na fungu maalum la fedha limetengwa..
“ Serikali imedhamiria kuipa uhuru tume, kuwapa sehemu nzuri
ya kufanyiakazi pamoja na nyumba za kuishi wana tume ambao wanatoka nje ya Dar
es Salaam,”amesema Sefue.
Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Cellina Kombani amesema umuhimu wa mabadiliko ya katiba ya
nchi ni mkubwa na wananchi wana matumaini na tume na ndiyo maana ilipotangazwa
hakuna malalamiko yaliyojitokeza.
Ameitaka tume hiyo ijipange vyema ili kuhakikisha inatoa
elimu ya katiba iliyopo ili wananchi waweze kutoa maoni ya katiba waipendayo
kwani muundo wa katiba hiyo ni jambo nyeti na lenye kuleta msisimuko.
“ Nina imani amani itatawala
na uwazi, kwani mchakato huu ni wa kuboreha mazuri, kuondoa mapungufu pia ni
kujipima tulikotoka na tuendako kwani nia si kuvunja umoja wetu bali mawazo ya
wananchi yataheshimiwa, “amesema Kombani.
Kombani ameongeza kuwa tume hiyo ndiyo nguzo ya mchakato wa
katiba mpya huku akisisitiza kufanikiwa au kutofanikiwa kutatokana na tume hiyo
kutekeleza majukumu yao
kwa kuwashirikisha wananchi bila ubaguzi.
“ Kazi hii inahitaji ushirikiano zaidi nafahamu kuna kipindi
mtakwazika na kutamani kuimbia kazi hii lakini mkiwashirikisha wananchi
mtafikia muafaka na hatimaye tutapata katiba inayostahili,”amesema Kombani.
Wakati huohuo, Waziri wa Katiba na Sheria Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar,
Abubakari Khamis Bakari amesema tume imepewa kazi ngumu ya kuwaelimisha
wananchi kwani wengi wao hawajui maana ya muungano.
Amesema ili katiba iwe yenye kukidhi haja ni muhimu wananchi
wakapewa fursa ya kutoa maoni ambayo yataisaidia tume hiyo kurahisisha kazi yao.
Amewatahadharisha wananchi kuacha kutumia mchakato huo kama njia ya kuibomoa nchi na badala yake fursa hiyo itumike kuunda
katiba yenye mantiki na inayokubaliwa na watu wote.
Hata hivyo hafla hiyo iliingiliwa na dosari baada ya
jenereta lililopo jirani na jengo hilo kulipuka
jana asubuhi na kusababisha umeme katika jengo hilo kukatika
hivyo kufanya hafla hiyo kuendeshwa bila vipaza sauti.
mwisho
No comments:
Post a Comment