Cheka,
Mashali kupima uzito
Na Mwali Ibrahim, Dar es Salaam
HOMA ya pambano la kuwania mkanda wa IBF/Afrika na gari aina
ya Noah lenye thamani ya Sh milioni 12 kati ya mabondia Francis Cheka na Thomas
Mashali, imezidi kupanda, baada ya mabondia hao leo kupima uzito kwa ajili ya mpambano huo
utakaofanyika kesho kwenye Ukumbi wa PTA, Dar es Salaam.
Tayari majaji na marefa kutoka nje ya nchi ambao wanakuja
nchini kusimamia mpambano huo, wamewasili nchini kwa ajili ya kumsaka bingwa
huyo, ambaye atakuwa kati ya Cheka, ambaye anatetea mkanda huo au Mashali anayeutaka
kwa mara ya kwanza.
Refa wa mpambano huo atakuwa John Shipanuka kutoka Zambia, huku majaji wakiwa ni Daudi Chikwanje kutoka Malawi, ambaye ndiye Katibu Mkuu wa Chama cha
Ngumi Malawi na ambaye anakuwa jaji namba moja, Steve Okumu wa Kenya, ambaye anakuwa jaji namba mbili na Ismail Sekisambu wa Uganda ambaye
anakuwa jaji namba tatu.
Na kwa upande wa msimamizi wa pambano hilo, atakuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Viwango na Ushindi wa Kamisheni ya Ngumi za
Kulipwa Tanzania (TPBC), Boniface Wambura, ambaye ni Ofisa Habari wa Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), atakayesimamia pambano hilo badala ya Rais wa IBF/Afrika
Mashariki na Kati, Onesmo Ngowi.
Kwa upande wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa
Tanzania (TPBO) ambao ni wa simamizi washiriki, Yassin Abdalah ‘Ostadh’ alisema
utaratibu na kanuni walizopanga kutumika katika mchezo huo ziko palepale, ikiwa
ni pamoja na kupima matumizi ya dawa za kuongeza nguvu na bangi ambapo mabondia
wote watapimwa na majibu kutolewa hapo hapo.
“Kama tulivyopanga awali, tunataka pambano hilo kuwa la kimataifa
kulingana na hadhi ya ubingwa wenyewe, hivyo mabondia hawa watapimwa matumizi
ya dawa hizo na endapo bondia atabainika kutumia atakuwa tayari ameishajitoa
katika mpambano na kumuacha mwenzie kutawazwa kuwa bingwa bila kupambana,”
alisema.
XXXXXX
Taifa Ngumi
kuanza mazoezi Mei 7
Na Mwali Ibrahim, Dar es Salaam
KIKOSI kipya cha Taifa cha Ngumi za Ridhaa kilichotangazwa
hivi karibuni na Kocha wa Mkuu wa ngumi hizo, Remmy Ngabo, kinatarajia kuanza
mazoezi rasmi Mei 7, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, kujinoa kwa
ajili ya mshindano ya Afrika yatakayofanyika Juni 20 hadi 30 nchini Mauritius.
Kikosi hicho cha mabondia 16 wakiwa na makocha tisa,
kilitangazwa hivi karibuni ambapo mabondia hao walichaguliwa kupitia mashindano
mbalimbali waliyoshiriki hivi karibuni.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la
Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Makore Mashaga, alisema kwa sasa wapo katika mchakato wa kuwaombea
ruhusa mabondia ambao ni wafanyakazi wa vyombo vya usalama, ili waweze kupata
nafasi ya kuanza mazoezi yao kwa pamoja na mabondia wengine.
“Mazoezi yatakuwa yanafanyika kila siku kuanzia saa tatu
asubuhi hadi saa sita mchana na kwa sasa tunajivunia kuwa na mabondia wengi
wenye umri mdogo na wakiwa ni mara ya kwanza kwao kuitwa timu ya Taifa, tuna imani
watakuwa na hamu kubwa ya kuiwakilisha vyema timu,” alisema.
XXXXXX
Lady Jay
Dee atuma salamu
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MSANII mahiri wa kike katika muziki wa kizazi kipya nchini,
Judith Wambura ‘Lady Jay Dee’, ametuma salamu zake kwa mashabiki wa muziki huo,
kwa kumuunga mkono tangu alipoanza kazi hiyo miaka 13 iliyopita.
Katika salamu zake hizo alizozitoa Dar es Salaam jana, Jay Dee,
alisema ameandaa sherehe
za miaka 13 zitakazoambatana na uzinduzi
wa albamu yake ya sita inayoitwa ‘Nothing But The Truth’, iliyo na jumla ya nyimbo
10, itakayofanyika Mei 31 mwaka huu.
Alisema
katika sherehe hizo pia kutakuwa na shoo ya nyimbo zote bora alizoshirikiana na baadhi ya
wasanii wenzake nchini.
“Nashukuru Mungu
tuko pamoja na pia nashukuru umma wa Tanzania kwa kuendelea kunipa ushirikiano
katika muziki wa Tanzania na kunipa nguvu mimi kama msanii.
“Nashukuru
vyombo vyote vya habari vinavyoshiriki kikamilifu kukuza na kulinda sanaa ya
Tanzania bila kujali maslahi binafsi,” alisema.
XXXXX
Skylight,
THT kupamba bonanza Mei Mosi
Na Humphrey Shao, Dar es Salaam
BENDI ya muziki wa dansi ya Skylight na kundi la wasanii
kutoka Nyumba ya Vipaji Tanzania (THT), wanatarajia kutoa burudani katika
bonanza la Mei Mosi, litakalofanyika katika viwanja vya Leaders Club, jijini
Dar es Salaam.
Bonanza hilo limeandaliwa na Clouds FM kupitia kipindi cha
Sports Extra kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mratibu wa bonanza
hilo, Shafii Dauda, alisema bonanza hilo
linatarajia kushirikisha jumla ya makampuni 14 yaliyotuma maombi ya kushiriki.
“Tulitangaza kupitia vyombo vyetu vya habari kama makampuni
yanayotaka kushiriki yajitokeze, hivyo makampuni yaliyojitokeza ni Shirika la Nyumba
la Taifa (NHC), TCC , Benki ya CRDB,
Simbanet, Shirika la Taifa la Hifadhi ya
Jamii (NSSF), Clouds Media Group, Fastjet, Umoja Water, Infinity, Tanesco na
NMB,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa nje wa Vodacom Tanzania, Salum
Mwalimu, alisema wameamua kushirikiana na Clouds kwa kuwa wao ni sehemu ambayo
wanafikia wateja wao wengi, hivyo hicho wanachofanya ni kwa ajili ya watu na
wao wapo kwa ajili ya watu.
XXXXX
Wasanii THT
kuachia Ugonjwa wa Moyo
Na Asteria Mdakirwa, Dar es Salaam
WASANII kutoka Nyumba
ya Vipaji Tanzania (THT), Saidi Christopher ‘Muki’ na Fred Felix ‘Fredwayne’
wanatarajia kutoa nyimbo nyingine mpya ijulikanayo kama Ugonjwa wa Moyo mwezi
ujao.
Wasanii hao awali walitoka na nyimbo ya Kibega, wameamua kuja
kivingine zaidi na wimbo huo uliotengenezwa katika Studio ya Surround Sound,
chini ya Emma The Boy.
Ugonjwa wa Moyo ni wimbo ulio katika hadhi na maadili ambayo
kila shabiki ataifurahia kutokana na kuimbwa katika lugha ya Kiswahili na Kikongo,
huku ikitengenezwa katika kiwango cha hali ya juu.
XXXXXXMWISHO.